.

.

.

.

Friday, February 20, 2015

JOSEPH KUSAGA AFUNGUKA KUHUSU CLOUDS MEDIA KUUZWA



TAHARUKI iliyosambaa jana kwenye mitandao kijamii juu ya kuuzwa kwa Clouds Media Group, inayomiliki Clouds FM, Clouds Tv na Choice FM, zimepata majibu baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Joseph Kusaga (pichani), kuibuka na kukataa habari hizo na kuziita ni uzushi wa kupuuzwa. 
Habari za kuuzwa kwa kampuni hiyo dhidi ya mfanyabiashara maarufu na kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Rostam Aziz, zilishika nafasi katika mitandao ya kijamii na hatimae kuzua usumbufu mkubwa kwa wafanyakazi, viongozi wa Clouds na Watanzania kwa ujumla.
 
Akizungumza leo asubuhi (jana) moja kwa moja katika kituo cha Radio cha Clouds FM, Kusaga alisema habari hiyo imetengenezwa na watu walioamua kupoteza muda wao katika mitandao ya kijamii, hali ya kuwa wapo wanaovuna fedha nyingi kwa kupitia njia hiyo ya mawasiliano (social media).
 
Alisema mara baada ya kuenea kwa habari hiyo, usumbufu mkubwa uliibuka kutokana na watu wenye mapenzi mema na kampuni hiyo kuanza kuhoji juu ya taarifa hizo kama zina ukweli, huku akisisitiza pia si kosa kuuza kwa kuwa ni jambo la kawaida katika mambo ya kibiashara.
 
“Clouds Media Group ni kampuni iliyoanzia chini kwa ushirikiano wa watu wengi, hivyo kuamua kuiuza kiholela ni jambo la kushangaza, ingawa pia si dhambi kufanya hivyo kwa mtu yoyote kwa sababu ni biashara kama zilivyokuwa biashara nyinginge.
 
“Naomba Watanzania wote wapuuze habari hizo na kuwataka wale wenzetu walioamua kuitumia mitandao vibaya waache na badala yake wajikite kufanya biashara kwa kupitia mitandao hiyo ambayo inalipa kama itatumiwa vizuri na si kueneza habari za kumuuzia Rostam ukizingatia kuwa hakuna kitu kama hicho na nina miaka sijakutana na mfanyabiashara huyo katika kikao chochote cha kujadili juu ya jambo hilo,” alisema Kusaga.
 
Aidha Kusaga alitumia muda huo kuwahakikishia Watanzania kuwa Clouds ni chombo huru kisichofungamana na chama chochote cha siasa, huku akisema kwamba katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu haki itatolewa kwa vyama vyote na wanasiasa wote.
 
“Huu ni mwaka mgumu, hivyo naomba niseme ikitokea suala la kuhoji au kuunga mkono siasa, basi haki itatolewa kwa wanasiasa wote, ukizingatia kwamba chombo chetu hakika chama cha siasa inachokiunga mkono kwa sababu zozote zile,” alisema Kusaga .
 
Katika hatua nyingine, Kusaga aliwataka Watanzania wote kuunga mkono juhudi za kupambana na dawa za kulevya, huku akisema sakata hilo linaathiri nguvu kazi ya Taifa, hususan kwa baadhi ya wasanii waliojiinga katika matumizi hayo ya dawa za kulevya.
 
“Sisi Clouds tunaungana na Watanzania wote wanaopambana juu ya matumizi mabaya ya dawa za kulevya, hivyo ni jukumu letu kubwa kuzidi kuelimisha jamii juu ya masuala hayo kwakuwa yanaathiri kwa kiasi kikubwa ndugu zetu, wakiwamo baadhi ya wasanii,” alisema.
 
Kwa mujibu wa Kusaga, jitihada nyingi zinawekwa katika kubuni mbinu mbalimbali za kuelimisha jamii katika mambo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba Tanzania inapiga hatua hatua katika nyanja za kielimu, kisiasa, kiuchumi na kijamii, huku akiwataka watu kufanya kazi bila kuchoka na si kupoteza muda kwa kueneza habari zisizokuwa na ukweli katika mitanda ya kijamii.
 
Clouds Media Group inayomiliki kituo cha Radio cha Clouds FM, Clouds Tv na Choice FM, ni moja ya makampuni ya wazawa yenye mafanikio makubwa, huku Watanzania wengi wakifuatilia matangazo katika vituo hivyo

No comments:

Post a Comment